DRC: Matamshi ya Obama kwa Afrika ni uongo mtupu.
Matamshi ya Rais Barack Obama wa Marekani kuhusu umuhimu wa kuimarishwa demokrasia katika nchi za bara la Afrika, yamekabiliwa na ukosoaji mkali kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Lambert Mendé, Msemaji na Waziri wa Mawasiliano wa nchi hiyo amesema kuwa, matamshi ya kiongozi huyo wa Marekani juu ya suala la demokrasia ni jambo ambalo viongozi wengi wa Magharibi wamekuwa wakilihitajia kwa miaka mingi.
Amesema kuwa, Rais Obama anataka kuonyesha kwamba, ni nchi pekee za Kiafrika ambazo zinatakiwa kusoma na kujifunza demokrasia na kupambana na ufisadi na kwamba suala hilo pekee ndilo litakalomaliza matatizo ya nchi za bara hilo.
Kwa upande wake Jean-Didier Elongo, mmoja wa viongozi wa chama tawala nchini Kongo DR, amesema kuwa, rais huyo wa Marekani kwanza haijui hali halisi ya nchi za Kiafrika, suala ambalo limemfanya kutoa maneno hayo bila kuzingatia.
Amesema kuwa, Rais Barack Obama anamaliza muda wake wa urais nchini Marekani huku akiwa hata haelewi uhalisia wa hali ya Afrika ambayo ana mahusiano nayo, hivyo katika hali kama hiyo hakutarajii kheri yoyote kutoka kwake.
Akihutubia mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia Rais Obama alisisitizia umuhimu wa kuimarishwa demokrasia na kupambana na ufisadi barani Afrika.
Post a Comment