Header Ads

NGELEJA ATAKA KUPIMWA KWA MAFANIKO YAKE YA NISHATI.

MBUNGE wa Sengerema William Ngeleja (CCM), amekitaka chama chake, katika kuteua mgombea rasmi wa urais wa kukiwakilisha kwenye uchaguzi mkuu ujao, wampime kwanza yeye kwa mambo 15 aliyofanya wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini.
Ngeleja ambaye ni miongoni mwa wagombea urais ndani ya CCM, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara pamoja na wana CCM waliojitokeza kumdhamini.
Alisema kiongozi bora anapaswa kupimwa kwa vigezo vya utendaji bora na uliotukuka kazini.
Alijinadi kuwa yeye wakati huo akiwa waziri wa nishati na madini alifanikiwa kufanya mambo kadhaa ya msingi ndani ya Serikali inayoongozwa na CCM ikiwemo uanzishwaji wa mchakato wa ujenzi wa bomba la gesi lenye urefu wa kilometa 542 kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Alisema wakati anateuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Nishati na Madini alikuta nchi ikiwa kwenye tatizo la mgawo wa umeme ulioathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi, lakini kwa juhudi zake na wafanyakazi wa wizara hiyo kwa ujumla walifanikiwa kumaliza tatizo hilo mwaka 2011.
Kwa mujibu wa mtia nia huyo katika kipindi chake cha uongozi akiwa waziri pia alifanikiwa kubuni mradi mkubwa wa umeme vijijini (REA) uliokuwa na lengo la kusambaza umeme kwenye vijiji vyote nchini ili Watanzania wanufaike na matunda ya nchi yao.
“Nimefanya mambo mengi sana ndani ya nchi hii nikiwa pale wizara ya nishati na madini…si rahisi kuzungumza mambo yote lakini ukweli ni kwamba wana CCM wanapaswa kuwapima watia nia wa kiti cha urais kwa vigezo na nadhani kwa sasa William Mganga Ngeleja anafaa kuwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania,” alisema Ngeleja.
Alitaja masuala mengine aliyofanya kuwa ni kudhibiti uchakachuaji wa mafuta uliokuwa unafanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, kutoa bei elekezi na bei ya kikomo ya mafuta nchini pamoja na kukarabati miundo mbinu ya shirika la umeme Tanzania (TANESCO) ambayo mingi ilikuwa katika hali mbaya.

Aidha Ngeleja ameendelea kusisitiza vipaumbele vyake vinne endapo atapewa ridhaa ya kuwa mgombea kuwa ni ujenzi wa uchumi imara, uimarishaji wa utawala bora, uimarishaji wa huduma za jamii pamoja na ujenzi wa miundombinu bora.HABARI LEO.

No comments